BODI YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI STADI YAZINDULIWA

 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mh. Prof. Joyce Ndalichako amezindua rasmi Bodi ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi inayoongozwa na Bw. Peter Maduki.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bodi hiyo, Prof. Ndalichako aliitaka bodi hiyo kutambua kuwa imebeba dhamana ya kusimamia eneo nyeti na muhimu sana kwa uchumi na maendeleo ya nchi, hasa katika kipindi hiki.
Alisema, Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi ni eneo muhimu sana katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii, kwani ndipo mahali panapozalisha nguvukazi yenye ujuzi kwa wingi zaidi, hivyo kuongeza ajira kwa vijana, kuongeza tija katika viwanda na kuboresha uzalishaji mali na huduma katika jamii.
Prof. Ndalichako aliongeza kuwa bodi hiyo imeundwa katika wakati mwafaka, ambapo itasimamia utengenezaji wa Mpango-Mkakati mwingine wa Tano na hivyo kusimamia utekelezaji wake tangu mwanzo na hivyo kuitaka bodi hiyo kusimamia vyema utengenezaji na utekelezaji wa Mpango-Mkakati huo ili uwe na mafanikio makubwa zaidi.
Aidha Waziri aliiagiza Bodi kuhakikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali inayosimamiwa na VETA ikiwemo ujenzi wa vyuo vipya na upanuzi wa vile vilivyopo pamoja na karakana za mafunzo unakwenda kwa kasi zaidi.
Vilevile Waziri aliagiza Bodi hiyo kupitia utaratibu wa udahili wa wanafunzi na kuona namna ya kuuboresha ili kuendana na mahitaji halisi ya sasa.
Awali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dr. Bwire Ndazi alisema mamlaka imedhamiria kuendelea kupanua wigo wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi ili kuyafikia makundi mbalimbali katika jamii; kusimamia ubora wa elimu kwa kuzingatia mahitaji ya soko la ajira na mwelekeo wa serikali ya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.
Naye Mwenyekiti wa Bodi hiyo Bw. Peter Maduki aliahidi kuwa Bodi yake itatekeleza majukumu waliyopewa na kuahidi kufanyia kazi maagizo ya Waziri na hivyo kuboresha utoaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini.
Wajumbe wa bodi hiyo ni Peter Maduki (Mkurugenzi Mtendaji, Taasisi ya kikristo ya huduma za Kijamii) Ally M. Ahmed (Mkurugenzi wa Ajira, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu), Onesmo P.S.Mbelle (Mkurugenzi wa Biashara Ndogondogo na za Kati, Wizara ya Viwanda,Biashara na Masoko), Winston M. Makere (Naibu Katibu Mkuu, RAAWU), Padre E. Mbegu (Naibu Katibu Mwandamizi, Baraza la Maaskofu Tanzania, Mary Shuma (Mkurugenzi wa Programu ya Maendeleo ya Wanawake, Jinsia na Watoto,Jumuiya Ya Kikristo Tanzania), Suleiman Lolila (Katibu mkuu, BAKWATA), Neema G. Mhondo (Mkurugenzi wa Huduma kwa Wananchi, Shirikisho la wenye Viwanda Tanzania), Rifai A. Mkumba (Mkurugenzi wa Rasilimali Watu, East African Cables (Tz) Ltd, Leah L. Ulaya kutoka RAAWU na Dr. Bwire Ndazi (Mkurugenzi Mkuu VET


Comments